KCSE Past Papers 2020 Kiswahili Karatasi ya 2 (102/2)

Kenya Certificate of Secondary Education

Kiswahili Karatasi ya 2

1. UFAHAMU:

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.(Alama 15)

Familia ya Mzee Mbula haikuwa kubwa wala haikuwa na watu wengi. Ilikuwa naye Mzee Mbula, mkewe na wanawe wawili; wote wamemaliza shule, wanasubiri milango ya heri iwaletee ajira. Mzee Mbula hakuwa na huo uzee vile. Alikuwa kajipakaza kutokana na kufahamu kwake kiasi si haba cha mambo ya kiasili. Tamaduni alizifahamu fika na desturi akazijua kwa kina.

Leo Mbula yuko kwake na mkewe, wapo ukumbini. Wanao wawili nao wapo pale pale kwenye kochi. Japo wamekaa wote mle ndani kwa muda wa yapata saa tatu ushei, hakuna asemaye na mwingine.

Unaweza kufikiri pana ugomvi. Lakini kwa hakika nyumba hii haijapata kushuhudia ugomvi wa aina yoyote baina yao.

Kila mmoja ana mlahaka mwema na wenziwe. Na hali hii ya kila mmoja kuwa kajivisha kimya si jambo litokealo kwa tukizi tu. Limejenga hema pale nyumbani, na wote limewavuta na kuwateka.

Mbula pale alipo anacheka bila kufahamu, na wote pale ukumbini wananyanyua kope kumtazama. Anacheka tena huku kichwa kaitunga chini kunako simu yake.

“Watu bwana…Dah! Hatari huyu bwana na viroja vyake.”

Mkewe, Mama Tola, anainua kichwa. Anamtazama kabla ya kutabasamu kisha anamdadisi, “Una nini Ba Tola? Mbona wacheka mwenyewe hapo? Tuambie cha mno nasi tukapata kucheka.”

Mbula hana habari kuwa yapo maswali aliyodondoshewa. Habari zile kwenye ile simu zimemtwaa na kumpeleka mbali kule; kule kwenye dunia iliyo mbali kabisa na ukumbi ule.

Baada ya muda kimya kinatawala na kila mmoja kujizika kwenye hamsini zake. Pale jikoni napo hamkani za jiko zilikiunguza chungu na kuyaacha matokeo yake kujitangaza kote Kote.

Harufu ile ilitanda kote na moshi mweusi kufanya kiwingu kilichochomokea dirishani huku kinachora njia ielekeayo mawinguni.

Kiasi kingine cha moshi huo kilijipenyeza kwenye nafasi ndogo chini ya mlango uelekeao ukumbini na kuitapakaza harufu yake iliyoranda sawia na moshi. Jirani mmoja pale mtaani alifika kujua kulikoni.

Alibisha na kabla aitikiwe alijitoma ndani na kuuliza.

“Jamani shemeji, hivi kuna nini humu?”

Wote mle ukumbini walishtushwa na kishindo kile, wakayatega masikio kama sungura aliyesikia vishindo vikimwelekea.

‘Ah shemeji, kumbe ni wewe! Hamna neno humu. Karibu ndani.”

Yule jirani alishindwa kuingia ndani na kuanza kuchemua. Moshi mle ukumbini ulikuwa umetamalaki ila waliokuwa ndani walikuwa hawatambui. Ndipo walipoisikia sauti ya yule jirani ikipenya ndani kutoka kule nje.

“Jamani moshi huo wote hamuuoni? Kinaungua nini?”

“Moshi?” Aliuliza Mbula.

“Maskini chungu changu!” Alitamka Mama Tola huku anakurupuka kuelekea jikoni ambamo alikaribishwa na wingu zito la moshi na mtatariko mkubwa wa chungu kilichokuwa kimekigeuza kile kitoweo kuwa mkaa mgumu ulioshikamana.

Mkewe Mbula alipotoka jikoni aliwataka Tola na Kola kumsaidia kufungua madirisha pale ukumbini ili upepo uingie na kuijengea nafasi hewa safi.

Wanawe hawakumsikia. Masikioni walikuwa wametia vidubwasha vya sauti walivyoviunganisha kwenye simu zao. Kila mmoja anafurahia alichokisikiliza na kukiona kwenye kioo cha simu chake.

Mama Tola alipandwa na hamaki, akawasogelea wanawe na kuwapokonya zile simu. Alikuwa tayari kuwakaripia alipoisikia sauti ya mumewe

“Yakimwagika hayazoleki. Yameshamwagika na kilichopo sasa ni kujizolea mafunzo. Sote tumeteleza na kudondokea mbali huko. Sote tumekuwa mbali huko zilikotupeleka simu zetu. Hatukujua tumetengana kiasi hiki. Imebaki kujirekebisha.”

Mkewe alimtazama kisha akawatazama wanawe. Polepole tabasamu iliupamba uso wake na baada ya muda midomo ilianza kumchezacheza kabla ya kicheko kikubwa kumtoka. Mbula naye alijikuta anachekeshwa na kicheko cha mkewe.

Alipogeuka aliwaona wanawe nao wanacheka. Hakujua kilichokuwa kinawachekesha lakini aliridhishwa na hali ile nzima japo hakujua kuwa nyumba nzima ilikuwa imepata marashi ya moshi wa kitoweo kilichoungua.

(a) Kwa kurejelea kifungu, fafanua matatizo manne yanayoweza kusababishwa na matumizi ya simu kwa familia. (alama 4)

(b) Eleza mambo matano yanayoonyesha kuwa familia hii ina mshikamano. (alama 5)

(c) Fafanua uhusiano uliopo kati ya familia ya Mzee Mbula na majirani. (alama 2)

(d) Thibitisha kuwa Mzee Mbula ni mtu anayejikuta baina ya usasa na ukale. (alama 2)

(e) Eleza maana za misamiati ifuatayo kwa mujibu wa kifungu. (alama 2)

i. Limejenga hema

ii. kuitapakaza

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali. (Alama 15)

Ukame ni tukio hatari la kimaumbile. Athari zake hutofautiana kutoka eneo moja hadi lingine. Kwa sababu hiyo. si rahisi Kuielewa dhana ya ukame; kwa hakika si rahisi kuifafanua dhana hii. Katika eneo la Bali, kwa mfano, isiponyesha kwa muda wa siku sita wenyeji huchukulia hali hiyo kuwa ukame japo kiasi hicho cha mvua ni kikubwa mno ikilinganishwa na Libya ambayo hupata kiasi kidogo cha chini ya milimita 180 ya mvua kwa mwaka.

Katika hali ya kawaida ukame hutokana na kipindi kirefu cha uhaba wa mvua hasa katika msimu mzima au zaidi. Uhaba huu wa mvua huweza kusababisha uhaba wa maji kwa shughuli, kundi au sekta fulani. Shughuli za binadamu huweza kufanya hali ya ukame kuwa mbaya zaidi. Shughuli hizo ni pamoja na kilimo, unyunyiziaji maji na ukataji wa miti.

Ni vigumu kubaini wakati mahususi ambao ukame huanza kwa kuwa kipindi hicho cha ukosefu wa mvua huwa cha mfululizo, na eneo huendelea kupata mvua iliyopungua kwa miezi au hata miaka. Mimea hukauka na wanyama hufa kutokana na ukosefu wa maji.

Ukame basi huwa hatari kwa maisha ya binadamu na viumbe wengine kwa kuwa huweza kusababisha njaa na kuyafanya maeneo kuwa majangwa.

Mbali na ukosefu wa mvua, ukame pia husababishwa na kiangazi. Kiangazi huongeza kiwango cha joto. Joto hilo huyafanya maji yaliyohifadhiwa kuwa mvuke haraka, hivyo kiwango chake kupungua.

Hali ya el ninyo pia husababisha ukame katika baadhi ya maeneo ambayo huwa hayana mvua. Upepo huivutia mvua mahali panaponyesha na kuliacha kame eneo ambalo halina mvua ya aina hii.

Hata katika maeneo yenye mvua ya el ninyo, kiangazi kikali huifuata na hivyo kusababisha ukame. Hali hii huitwa la nina. Mambo yanayotokana na mabadiliko ya hali ya anga ulimwenguni pia yanaweza kuchangia hali ya ukame. Ongezeko la joto duniani linafanya hali ya ukame kuwa mbaya zaidi.

Ukame una madhara chungu nzima kwa binadamu. Madhara hayo huweza kuwa ya kiuchumi, kimazingira au hata kijamii. Ukame husababisha kupungua kwa mimea na mavuno. Huweza pia kutokea dhoruba za mchanga. Dhoruba hizi hutokea palipo na jangwa. Ukosefu wa maji ya kunyunyizia mimea husababisha njaa na magonjwa kama vile utapiamlo yanayotokana na ukosefu wa lishe bora.

Makazi ya wanyama wa nchi kavu na wale wa majini pia huathiriwa vibaya. Hali kadhalika, ukame husababisha uhamaji. Hii inamaanisha kuwa jamii huweza kutoka katika makazi asilia na wakati mwingine huweza hata kuwa wakimbizi.

Ukame husababisha ukosefu mkubwa wa maji. Ukosefu huu huwa na athari hasi kwa maendeleo ya viwanda kwa kuwa vingi huhitaji kiasi kikubwa cha maji. Juu ya hayo, maji huhitajika katika kuzalisha umeme. Umeme una matumizi mengi katika viwanda, nyumbani, afisini na hata hospitalini. Ukosefu wa umeme basi huwa ni tatizo kuu.

Aidha, ukame unajulikana kusababisha uhasama wa kijamii. Jamii huweza kuzozana na hata kupigana kutokana na uhaba wa rasilimali za asili kama vile chakula na maji. Pia mioto mikubwa huweza kuenea haraka wakati wa ukame na hivyo kusababisha vifo vya binadamu na wanyama na uharibifu wa rasilimali nyingine.

Ingawa ukame husababisha madhara mengi, binadamu wanaweza kujikinga kutokana nao kwa kupunguza makali ya ukame. Jambo la kwanza wanaloweza kufanya binadamu ni kuhifadhi maji. Maji ya mvua yanafaa kuhifadhiwa katika mabwawa na mapipa.

Haya yanaweza kutumiwa wakati wa ukame hasa katika kukuza mimea. Mkakati mwingine ni kutumia mbinu za kupunguza chumvi na kemikali nyingine zilizomo kwenye maji ya bahari ili yaweze kutumika katika unyunyiziaji wa mimea. Hili litapunguza tatizo la ukosefu wa chakula.

Pia ni muhimu kufanya utafiti kuhusu hali ya anga ili kupanga na kuweka mikakati ifaayo kukabiliana na hali hiyo.

Ni muhimu kuwa na mipangilio mizuri ya matumizi ya ardhi. Mathalani upanzi wa mimea itakayozuia mmomonyoko wa udongo, kubadili aina ya mimea inayokuzwa sehemu fulani pamoja na upanzi wa mimea isiohitají mvua nyingi katika maeneo kame ni hatua mwataka.

Aidha, ni vizuri kupunguza matumizi ya maji hasa katika mazingira ya nyumbani kwa mfano tunapofua na kuosha. Njia nyingine ya kukabiliana na tatizo hili ni kusafisha maji yaliyotumiwa ili kuyatumia tena.

(a) Kwa maneno 50, eleza visababishi vya ukame kwa mujibu wa taarifa. (alama 4; 1 ya mtiririko)

Matayarisho

Nakala Safi

(b) Fupisha ujumbe wa aya ya tano hadi saba kwa maneno 70. (alama 6; l ya mtiririko)

Matayarisho

Nakala Safi

(c) Eleza masuala ambayo mwandishi ameibua katika aya mbili za mwisho kwa maneno 60. (alama 5; 1 ya mtiririko)

Matayarisho

Nakala safi

3. MATUMIZI YA LUGHA: (Alama 40)

(a) Andika maneno yenye miundo ifuatayo: (alama 2)

(i) Kipasuo ghuna cha midomoni, irabu ya chini, kati, kipasuo sighuna cha ufizi, irabu ya juu mbele

(ii) Nazali ya ufizi, kipasuo ghuna cha kaakaa laini, irabu ya juu, nyuma, irabu ya nyuma wastani

(b) Bainisha silabi zinazowekwa shadda katika maneno yafuatayo: (alama 1)

(i) waliotusifia

(ii) sherehekea

(c) Andika sentensi ifuatayo katika umoja. (alama 1)

Nyua walizojenga hapa zimesaidia kukabiliana na wahalifu hao.

(d) Geuza sentensi ifuatayo katika hali ya udogo. (alama I )

Mbuzi huyo wake ana ngozi laini.

(e) Tunga sentensi moja yenye nomino dhahania na kivumishi kimilikishi. (alama 1)

(f) Andika upya sentensi zifuatazo kulingana na maagizo.

(i) Maafisa hao walipewa uhamisho. Maafisa wengine hawakupewa uhamisha (Unganisha kuunda sentensi ambatano.) (alama 2)

(ii) Hadithi hiyo ilitungwa vizuri ikawavutia wengi. (Badilisha vitenzi vilivyopigiwa mstari kuwa nomino.) (alama 2)

(iii) Tunda halitaoshwa vyema. Tunda halitalika. (Unganisha kuwa sentensi moja kwa kutumia ‘po’.) (alama 2)

(iv) Kengewa alitoa ahadi. Wengi waliiamini ahadi hiyo. (Unganisha kuwa sentensi moja inayoanza kwa: Ahadi.) (alama 2)

(g) Tunga sentensi ya masharti inayoonyesha kwamba kitendo kilifanikiwa kutokana na kufanikiwa kwa kingine. (alama 2)

(h) Tunga sentensi yenye kishazi kirejeshi ambacho ni kielezi. (alama 2)

(i) Ainisha maneno yaliyopigiwa mstari katika sentensi ifuatayo:

(alama 3)

Mwenyewe hakuwa amekupa ruhusa kuitumia.

(j) Akifisha sentensi ifuatayo: (alama 2)

Mwanangu akasema Neema huku amemkazia macho huoni unamtia mwenzako wasiwasi

(k) Andika maneno yenye mofimu zifuatazo: (alama 2)

(i) Umoja (ngeli ya U-1), mzizi, kiishio

(ii) Kikanushi, kiambishi ngeli (Kl-VI umoja), mzizi, kauli tendeka, kiishio

(l) Tunga sentensi yenye muundo ufuatao: (alama 2)

KN (N+ R H) +K T(T+ E)

(m) Andika sentensi ifuatayo katika hali ya kukanusha. (alama 1)

Ngoma hizo zilihifadhiwa ili ziuzwe mjini.

(n) Andika sentensi ifuatayo katika wakati uliopita hali ya mazoea. (alama 2)

Bili atawashauri vijana kuhusu umuhimu wa michezo.

(o) Andika sentensi ifuatayo katika kauli ya kutendesha kwa kuzingatia maneno yaliyopigiwa mstari. (alama 2)

Alimfanya Tindi anywe pombe ikamfanya alewe.

(p) Tunga sentensi ukitumia mzizi, -ingine kumaanisha “baadhi ya”. (alama 2)

(q) Hewala ni kwa kukubaliana na jambo,…………….ni kwa kutaka kitu kinusurike na ……………ni kwa aliyefanya vyema katika jambo. (alama 1)

(r) Zito ni kwa jepesi,………….ni kwa choyo, na ……….. ni kwa kali. (alama 1)

(s) Andika visawe vya kauli zilizopigiwa mstari. (alama 2)

Musei alikumbwa na malatizo mengi lakini hakukata tamaa. (t) Tunga sentensi moja kubainisha maana mbili za neno: zima. (alama 2)

4. ISIMUJAMII: (Alama 10)

Umewahutubia wanaeneobunge lako kuwaomba wakuchague kuwa mbunge wao. Hata hivyo, umegundua kwamba hujafanikiwa kuwavutia upande wako. Fafanua sifa kumi za lugha ambayo ungetumia kuwavutia. (alama 10)

(Visited 415 times, 1 visits today)
Share this:

Written by