KCSE Past Papers 2020 Kiswahili Karatasi ya 3 (102/3)

Kenya Certificate of Secondary Education Kiswahili Karatasi ya 3

Jibu maswali manne pekee.

Swali la kwanza ni la lazima.

Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki; yaani: Riwaya, Tamthilia, Ushairi na Fasihi Simulizi.

Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.

Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

SEHEMU A: HADITHI FUPI

A. Chokocho Na D. Kayanda: Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine

1. Lazima

D. Kayanda: “Mwalimu Mstaafu”

(a) “Naomba radhi mfawidhi … lakini nadhani ni jambo la busara kutokitia mchanga kitumbua .. . “

(i) Eleza muktadha wa dondoo hili .(alama 4)

(ii) Bainisha toni ya dondoo hili. (alama 2)

(iii) Kwa kurejelea hadithi hii jadili kwa kutoa hoja kumi namna mhusika Jairo alivyokitia kitumbua mchanga. (alama 10)

(b) Bainisha vipengele vya kimtindo katika dondoo lifuatalo: (alama 4)

“Alijaaliwa mvi nyeupe zilizojianika kwenye kichwa chake kidogo kilichosimama jadidi kwenye shingo yake nyembamba. Alijaaliwa mvi kwa vile zilikuja mapema wakati akiwa bado ana umri wa miaka thelathini. Watu wakasema hekima hiyo kutabasuri huko. Kwa hiyo, hakujisumbua kujipaka rangi nyeusi kuung’ang’ania ujana uliotishia kumwondoka mapema … mvi zimemkaa kwa haiba kama theluji … “

SEHEMU B: RIWAYA

A. Matei: Choi la Heri

Jibu swami la 2 au la 3

2. (a) “Mara moyo unaanza kumwenda mbio na vipapasio vya akili yake kusimama wima. Anajihisi kama anayetarajia kuanza kinyang’anyiro kikali cha upiganaji masumbwi.

Kwa mbali anasikia mbisho hafifu … Anatoka nje kwenda kuitikia mbisho huu … Mara anasikia moyo wake ukimwambia, “Yako ya arobaini imefika,” …

(i) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)

(ii) Jadili aina mbili za taswira katika dondoo hili. (alama 2)

(iii) Bainisha vipengele vingine vinne vya kimtindo katika dondoo hili. (alama 4)

(b) Jadili umuhimu wa mandhari katika kuijenga riwaya hii kwa kurejelea kituo cha afya cha Mwanzo Mpya. (alama 10)

3.(a) Changanua mtindo katika kifungo kifuatacho:(alama 8)

Wakati kama huu Mwangeka angejitanua kifua na kusema. “Mimi ni mwana wa mhunzi, na bila shaka wa mhunzi asiposana huvuvia.

Babangu hakuna linalomshinda katika uwanja wa upasuaji. Ni kama yule mbabe wa kivita aliyepigana na Akavi kuwakokoa mifugo wa ukoo wetu kutokana na kutekwa na jamaa hawa ambao siku hizo wakiamini ndio waliotunukiwa na Manani jukumu la kuwamiliki ng’ombe wote.

Baba huniambia kuwa mara nyingi huwafufua maiti katika chumba cha wagonjwa mahututi, akawatoa kwenye mashine na kuwarejeshea uhai, jamaa zao wakitazama hivi hivi! Hilo usilione dogo. Tet! Baba si tofauti na huyo Fumo Liyongo tuliokuwa tukihadithiwa na nyanya. Ati bwana huyu angeweza kuinua tani ngapi vile za chuma?”

“Mia moja!” Mwangemi angemkumbusha mwenzake kila mara.

(b) Kwa kurejelea kisa kinachosimuliwa kuhusu Mwangeka,Mwangemi na babu yao,jadili mchango wa familia katika kuendeleza desturi za kijamii.

SEHEMU C: TAMTHILIA

P. Kea: Kigogo

Jibu wali la 4 au la 5

4. “Nilijua ninapoanza, nilijua ninawapunja, nilijua ninawadhuru… lakini nilimezwa na tamaa”

(a) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)

(b) Bainisha vipengele viwili vya kimtindo katika dondoo hili. (alama 4)

(c) Fafanua umuhimu wa mzungumzaji katika kuvijenga vipengele vifuatavyo vya tamthilia hii.

i. Ploti

ii. Maudhui

5.(a) Jadili mchango wa wasomi katika hali ya maisha ya Wanasagamoyo (alama 10)

(b) Fafanua umuhimu wa mazungumzo kati ya Majoka na Daktari katika kujenga tamthilia ya Kigogo.(alama 10)

SEHEMU D: USHAIRI

Jibu swami la 6 au la 7

6. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

Mruka juu kipungu, hurejea ardhini

Yasemwa tangu tangu, zamani hizo zamani

Ukweli jua mchungu, hili mja ubaini

Mpanda ngazi jamani, hakwei ili kushuka.

____________________________________________________ Muhali hili nasema, mpanda ngazi kushuka

Utabaki kutazama, kama ataporomoka

Hapo juu kagandama, kileleni amefika

Mpanda ngazi jamani, kurudi chini hawezi.

____________________________________________________ Kurudi chini hawezi, hili jambo muhali

Ameotesha makwezi, apania kwenda mbali

Angani ndio makazi, kuanisi kila hali

Mpanda ngazi jamani, kushuka chini haramu.

______________________________________________________ Kushuka chini haramu, hili bado nakariri

Twabaki kumhukumu, mkwezi huyu mahiri

Usingoje kwa hamumu, zapita nyingi dahari

Mpanda ngazi jamani, amebaki kileleni.

_________________________________________________________ Amebaki kileleni, hukohuko anaketi

Daima yu furahani, hapati shida katiti

Walo chini mashakani, walia zao nyakati

Mpanda ngazi jamani, amepanda akapanda.

___________________________________________________________ Amepanda akapanda, walio chini wa chini

Umpinge ukipenda, ila hili libaini

Mpanda ngazi kapanda, harudi tena badani

Mpanda gazi jamani, hatashuka kwa hiari.

______________________________________________________________________ Hatashuka kwa hiari, jinsi anavyoanisi

Wala haoni hatari, katu hana wasiwasi

Anaishi kwa fahari, ni nyofu yake nafasi

Mpanda gazi jamani, hakwei ili kushuka

___________________________________________________________________ Hakwei ili kushuka, kuacha yake makao

Ameshika kwa hakika, mashiko penye mafao

Amepanga kaka kaka, kuchuma mengi mazao

Mpanda ngazi jamani, kuija chini hashuki.

___________________________________________________________________ Kuija chini hashuki, mti ungaporomoka

Tumpige kwa mikuki, ngawiraye kumpoka

Atahapa haki haki, si halali kwa hakika

Mpanda ngazi jamani, harudi katu harudi.

____________________________________________________________________ Harudi katu harudi, kurudi chini tulipo

Apigwe pigo ja radi, atabaki papo hapo

Bado azidi kaidi, kuapa kila kiapo

Mpanda ngazi jamani, hakwei ili kushuka.

(b) Eleza aina nne za taswira zinazojitokeza katika shairi hili. (alama 4)

(c) Bainisha aina tatu za urudiaji zilizotumiwa katika shairi hili. (alama 3)

(d) Huku ukitoa mifano, onyesha mbinu mbili ambazo mshairi ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi. (alama 2)

(e) Bainisha mbinu zifuatazo za kimtindo katika shairi hili:

(alama 3)

(i) Tanakuzi

(ii) Chuku

(iii) Sitiari

(f) Eleza muundo wa ubeti wa tisa na kumi.

(alamu 2)

7. Soma Shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

U wapi ujana wangu, na madhubuti ya nia?

Niko hapa peke yangu, ujana umepotea

Umeanacha na machungu, mambo niliyozoea

Kuwa na uwezo wangu, leo hayawezi kuwa

Afya ya ujana wangu, nayo imeshika njia,

Siku za ujana wangu, nazo sizioni pia,

Nadhari sasa si yangu, tazama hii dunia!

__________________________________________________ U wapi ujana wangu, ubingwa na mazoea?

Ndugu za jamaa zangu, na watu niliojua,

Wamehama ulimwengu, ni pweke nimebakia

Nguvu wanazo wenzangu, sasa wanazitumia

Nikishikacho si changu, ajabu hii dunia.

Hutia kizunguzungu, wakati wa kuchungua

Kama hukumbuki Mungu, kufuruni utakuwa.

__________________________________________________ U wapi ujana wangu, na maringo ya tabia?

Hamna kinywani mwangu, jino lililobakia,

Na laini gumu kwangu, sina cha kutafunia

Kitamu sasa kichungu, hata kama ni halua

Kama ningefungwa pingu, sina la kufurahia

Katika maisha yangu, nimebaki na fadhaa

Kama fumbo ulimwengu, na watu wazuzuliwa.

(a) Bainisha kwa hoja tano kinyume kinavyojitokeza katika shairi hili. (alama 5)

(b) Eleza muundo wa shairi hili. (alama 4)

(c) Eleza aina nne za taswira katika shairi hili. (alama 4)

(d) Onyesha mifano ya mbinu zifuatazo katika shairi hili: (alama 4)

(i) Kweli kinzani

(ii) Tashihisi

(iii) Tasfida

(iv) Usambamba

(e) Bainisha nafsineni katika shairi hili. (alama 1)

(f) Eleza toni ya shairi hili. (alama 2)

SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI

8. Soma Kiungu ufutao Kisha ujibu maswali.

Zamani sana Sungura na Fisi walikuwa marafiki wa kufa kuzikana. Mjukuu wangu sijui kama umewahi kuuwazia urafiki wa aina hii, ule wa mmoja wao akijikwaa dole anayeuhisi uchungu wenyewe ni mwenzake.

Siku moja walialikwa karamuni na Tumbili. Marafiki hawa waliafikiana waandamane asubuhi na mapema.

Hata hivyo, Fisi alipofika nyumbani kwake moyo wake ulimrai.”Ndugu, wewe unajua mambo ya akutanguliaye chanoni hukuzidi tonge na atanguliaye kisimani hunywa maji maenge? Itakuwaje umngojee Sungura na hali kimo chake ndicho hicho? Hata akafika amechelewa atakula shibe yake, wewe unahitaji kutwa nzima kulijaza tumbo lako kuza. Wewe jihimu mapema, huyu mwenzako atakufuata.”

Asubuhi na mapema Fisi alishika tariki … guu mosi, guu pili… guu mosi, guu pili … hadi kwa Tumbili Harufu nzuri ya mapochopocho ilihanikiza hewa; harufu ambayo ilimfanya Fisi kuchezesha midomo yake hivi na mate kudondoka ndo ndo ndo! Fisi alifika karamuni na kuchukua nafasi katika viti vya mbele asije akapitwa na chochote.

Nyuma kule Sungura alipitia kwa Fisi lakini hakumpata.

“Lo, kiumbe huyu!” Sungura alimwuliza Fisi kimoyomoyo, “utaacha lini tabia hii ya usaliti?” “Lazima nikukomeshe!”

Sungura alipofika karamuni alikaa kule nyuma akiwazia la kufanya. Fisi ambaye hakuwa na mwao na yaliyokuwa akilini mwa Sungura alimwendea na kumwambia.

“Ndugu yangu, mtu huhifadhi akipatacho. Sijui kama nitawahi kuambulia shibe ya aina hii. Je, waonaje tukichukua baadhi ya vyakula hivi tupeleke nyumbani?”

Sungura alimwambia. “Hamna haja kujidhalilisha. Njia mufti ya kuhakikisha hutaona njaa tena ni kuhifadhi kilicho tumboni. Basi nitatumia ujuzi wangu wa utabibu kukusaidia kukitunza chakula tumboni. Fisi alikubali haraka.

Fisi alilia kwa maumivu makali lakini alipofikiria kuhusu kile chakula slivumilia huku mwili mzima unamtetema. Sungura alikamilisha rnpango wake na kutwaa tabasamu la ushindi.

Basi mjukuu wangu, Sungura aliutwaa uzi na sindano ambayo alikuwa kahifadhi kwenye kijaluba akaanza kuupitisha ule uzi polepole kwenye msamba wa fisi. Fisi alilia kwa maumivu makali lakini alipofikiria kuhusu kile chakula alivumilia huku mwili mzima unatetema. Sungura alikamilisha mpango wake na kutwaa tabasamu la ushindi.

Baada ya muda, Fisi alirejea kubugia sahani za vyakula na mifupa bila kufanya nadhari. Polepole, maumbile yalianza kudai haki, naye akatanabahi kwamba Sungura alikuwa kamnyima uwezo wa kuyatosheleza maumbile haja. Aliangaza macho huku na kule, asimwone Sungura. Alijikokota mithili ya ng’ombe anayechungulia kaburi hadi kwa Sungura.

Alimsihi Sungura amwondolee udhia huu lakini Sungura alikataa katakata, akamwambia “Jikune ujipatapo.” Na kweli Fisi alijikuna ajipatapo. Kabla Sungura hajafumba jicho, alisikia kilio cha kite, kisha mpasuko mkubwa Sungura aliangua cheko kubwa la stihizai na kumsukuma Fisi kutoka nyumbani kwake huku amefunika mianzi yake ya pua kwa viganja. Huo ukawa mwisho wa urafiki wa Sungura na Fisi. Tangu wakati huo, Fisi yumo mbioni kumtafuta Sungura iii amwadhibu.

Hadithi yangu imeishia hapo. Naomba ng’ombe wangu wafaidi nyasi za kijani na wako wafe kwa kiangazi.

(a) Onyesha kwa nini hii ni ngano ya usuli. (alama 2)

(b) Fafanua vipengele kumi vya kimtindo ambavyo fanani ametumia kufanikisha uwasilishaji wake. (alama 10)

(c) Eleza umuhimu wa fomyula ya mwisho katika ngano hii. (alama 3)

(d) Wewe ni kati ya wanaotambiwa ngano ya aina hii. Fafanua mambo matano ambayo wewe na wenzako mnaweza kuchangia wakati wa utambaji. (alama 5)

 

(Visited 809 times, 1 visits today)
Share this:

Written by